MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo inatarajia kutoa hukumu ya Kesi ya Uhujumu
Uchumi na Kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, inayomkabili
aliyekuwa Balozi wa Tanzania, nchini Italia Profesa Costa Mahalu na
Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.
Profesa
Mahalu na Martin wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu
uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, katika
mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Hukumu
ya kesi hiyo iliyokuwa ikinguruma mahakamani hapo kwa miaka kadhaa
sasa, inatarajiwa kusomwa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Ilvin Mugeta ambaye amekuwa akiisikiliza.
Awali,
hukumu hiyo ilipangwa kusomwa Julai 11, mwaka huu lakini iliahirishwa
kutokana na Hakimu Mugeta kukabiliwa na majukumu mengine. Kesi hiyo
iliahirishwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na kupanga kuwa hukumu
hiyo itasomwa leo.
Kiongozi
wa jopo la mawakili wa washtakiwa hao, Mabere Marando alisema jana
kwamba anaamini kesi hiyo ambayo imechukua muda mrefu, leo inafikia
mwisho kwa Mahakama kutoa hukumu.
Hata
hivyo, hakutaka kuizungumzia kwa undani hukumu ya leo badala yake
alisema kuwa wanachosubiri ni kuona itakavyokuwa, ila wako tayari kwa
matokeo yoyote.
“Sisi
tunasubiri kuona hukumu ya Mahakama, kwani imekuwa ikisubiriwa sana.
Kama akiachiwa tutafurahi na tutakunywa wine (mvinyo) usio na kilevi
kama akifungwa basi tutapiga magoti kumwombea,” alisema Marando kwa
utani huku akicheka.
Alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho ni wa Mahakama na kwamba mambo mengine yatafuata baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo.
Kwa
upande wake, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alisema katika makosa
kama hayo yanayowakabili washtakiwa hao, ikiwa watapatikana na hatia
adhabu yake inaweza kuwa kifungo kisichozidi miaka 15 jela.
Alisema
kwa mujibu wa Kifungu cha 60 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Kifungu
kidogo cha pili, Mahakama inaweza kutoa amri nyingine ikiwamo mshtakiwa
kulipa fidia.
Hukumu
ya kesi hiyo leo inasubiriwa kwa shauku si tu na Profesa Mahalu na
wenzake ambao wangependa kujua hatima yao, bali pia na umma wote wa
Watanzania ambao umekuwa ukiifuatilia kwa muda wote.
Wakati
wa utetezi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa
jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake, alipanda kizimbani na
kumtetea Profesa Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa
jengo hilo ulifuata sheria.
Mkapa
katika ushahidi wake wa utetezi licha ya kudai kuwa mchakato huo
ulifuata taratibu na kwamba ni yeye aliyebariki, pia alimmwagia sifa
kedekede Profesa Mahalu akidai kuwa ni kiongozi mwadilifu na mwaminifu
katika historia yake ya utumishi wa umma.
Akiongozwa
na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Alex Mgongolwa,
Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na malipo yake kwa
kuwa lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
Wakati
upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwapo
kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa
aliifahamu mikataba yote hiyo na malipo kufanyika kupitia akaunti mbili
tofauti.
Alieleza
kushangazwa kwake kusikia kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati
huo, Martin Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa hakujua mchakato
wa ununuzi wa jengo hilo, akisema hajui ni kwa nini Lumbanga alisema
hivyo.
Mbali
na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo wakati wa
ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa waziri wake,
Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Ujenzi na ile ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Alidai
kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini
ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake. Alisema taarifa
iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete bungeni juu ya
ununuzi wa jengo hilo ni sahihi.
Pamoja
na mambo mengine, taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa
kwa Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa
wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG).
“Maneno
hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi,” alisema Mkapa na kuongeza
kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa
sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki
akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano.
Akijibu
swali la Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa
CAG kuhusu ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa hajawahi kupokea
malalamiko hayo.
Akijibu
swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni
kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia mikataba miwili, Mkapa
alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa anahitaji ni kupata jengo.
Akijibu
swali kwamba kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa kwa mikataba
miwili lilikuwa ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake, Mkapa alijibu:
“Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na
nimepata nyumba, nasema Alhamdulillah.”
Pia
Mkapa alisema anamshangaa wakili wa Serikali kudai kuwa pesa hizo
kulipwa kwa awamu mbili kunaonyesha kwamba Profesa Mahalu alikuwa na
lengo za kuzichukua na kuzitumia kwa masilahi yake... “Mimi nitashangaa
sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa (Mahalu)
mimi namwamini.”
Utetezi wa Profesa Mahalu
Katika
utetezi wake, Profesa Mahalu alikana mashtaka hayo na kudai kuwa
alipofika katika ubalozi huo alikuta ofisi hizo zikiwa na hali mbaya
hali iliyosababisha kutoa fedha zake za mfukoni na kununua samani zenye
hadhi ya ofisi ya ubalozi.
Alisema
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Kikwete
pia alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya na
kwamba aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri
ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.
Alisema
mwanzoni mwa Juni, 2001 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alimpigia simu
akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila
ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge.
Alidai
kuwa Katibu Mkuu alimtaka yeye na maofisa wengine wa ubalozi kuanza
kutafuta majengo. Alisema baada ya hapo aliwaagiza maofisa wake kwenda
kutafuta majengo ndani na nje ya Jiji la Rome kwa ajili ya kulinunua.
Martin
katika utetezi wake alidai kuwa, Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali
hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na
jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.
Akiongozwa
na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili, Grace
alidai: “Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, Balozi Mahalu mashtaka yote sita
yanayomkabili hakuyatenda, aliwasilisha mikataba miwili kama taarifa
iliyofanyika kihalali.”
Pia
Martin alihoji sababu ya upande wa Jamhuri kutomleta mmiliki wa jengo
hilo la ubalozi kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuulizwa juu ya ununuzi
wa jengo hilo akidai walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi.
Chanzo: Mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment